UTEKELEZAJI WA MIRADI MIKUBWA YA MAGEUZI YA KIBIASHARA
Kampuni ya Simu Tanzania
(TTCL) ni kampuni inayotoa huduma bora
kwa makampuni makubwa ndani na nje ya Tanzania, pia imeunganisha nchi yetu na
nchi za jirani Rwanda, Burundi, Malawi, Kenya, Uganda na Zambia kupitia Mkongo
wa Taifa wa Mawasiliano. Nchi hizo zimeungwa kupitia TTCL kwenda kwenye mikongo
ya baharini ya SEACOM na EASSy pamoja na Kituo cha Mawasiliano ya Intaneti (IP
PoP) cha TTCL.
Pia,
inaunganisha taasisi za fedha, taasisi
za afya na hospital, Wizara na taasisi zake, watoa huduma za intaneti (ISPs),
watoa huduma za simu (telecom operators) ni baadhi ya wateja wetu wanaonufaika na huduma zetu
mbalimbali tunazozitoa. Na hii inatokana na kuwa TTCL ni Kampuni pekee yenye miundombinu ya kuaminika, uhakika,
yenye ubora na iliyosambaa nchi nzima.
Ili kupanua wigo
wa matumizi ya mawasiliano ya simu na TEHAMA nchini nzima, Kampuni iko kwenye
utekelezaji wa miradi mikubwa ya mageuzi ya kibiashara, kiufundi, masoko na
mauzo. Utekelezaji wa miradi hii ulianza
mwaka 2014 na unatekelezwa kwa awamu, hii ikiwa ni awamu ya kwanza na tunategemea
kumaliza awamu zote mwaka 2017. Kukamilika
kwa miradi hii, italeta mabadiliko makubwa katika utoaji huduma kwa wananchi
ambapo itaiwezesha TTCL kuwa kampuni inayotoa huduma bora zaidi na kwa bei
nafuu.
Katika eneo la
ufundi tuna miradi ambayo inalengo la kuboresha mitandao yetu na huduma
zinazotokana na mitandao, kupanua mitandao na kuhakikisha huduma za TTCL
zinapatikana nchi nzima na kwa bei nafuu. Maboresho hayo, yatawezesha upatikanaji wa huduma
za simu za mezani, mkononi pamoja na huduma za intaneti zenye ubora na kasi ya hali ya juu kwa wateja wetu nchi
nzima.
Katika kufanikisha hilo, TTCL na Kampuni ya MS
Huawei Technologies ya China siku ya leo
zinaingia mkataba ambao unalenga katika kujenga, kupanua na kuboresha mtandao
wa TTCL wa simu za mezani, mkononi pamoja na Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) ambapo miradi hiyo itagharimu zaidi ya kiasi cha dola za
kimarekani 182. Awamu ya kwanza ya mradi
huu inategemea kukamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu, 2015.
Miradi ambayo
iko kwenye mkataba itahusisha ujenzi wa mtandao wa teknolojia ya kisasa ya 4G Long
Term Evolution (LTE), 3G - UMTS pamoja na 2G- GSM, teknolojia hizi zitasaidia
Kampuni kupanua na kuboresha huduma zake nchi nzima na katika ubora wa hali ya
juu. Teknolojia hizi zitatoa huduma bora
ya sauti na intaneti (data) yenye kasi zaidi.
Mkataba huu pia
unahusisha ununuzi wa mitambo kwa ajili ya kupeleka mawasiliano vijijini chini
ya mpango wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF). TTCL imeshinda zabuni ya
kupeleka mawasiliano katika kata 69 zinazojumuisha vijiji zaidi ya 400 vyenye
wakaazi zaidi ya laki tano. Chini ya mradi huo UCSAF itaipatia TTCL Dola za
Marekani milioni kumi kujenga miundo mbinu ya mawasiliano katika Kata hizo.
Mkataba wa TTCL
na Huawei ni moja ya juhudi zinazofanywa na Kampuni katika kutekeleza mikakati
endelevu ili kuboresha na kupanua upatikanaji wa huduma nafuu za mawasiliano ya
simu na intaneti nchi nzima. Aidha, mikakati hii inaunga mkono juhudi za serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
katika kuhakikisha huduma za simu na intaneti zinawafikia watanzania
waliopo vijijini na mjini.
Hivyo, tunapenda
kuwahakikisha watanzania na wateja wetu kuwa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) iko imara, na imejipanga kimkakati katika
kuhakikisha inaendelea kutoa huduma endelevu, bora na nafuu kwa wateja wetu wa
ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
TTCL huleta watu Karibu
Comments
Post a Comment